Jumatatu , 17th Jun , 2019

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Ndugu Humphrey Polepole, amesema Vijana wa CCM waendelee kuwa na ujasiri, umoja na mshikamano katika kulinda na kutetea maslahi ya Chama na Taifa pamoja na kuepuka vikao visivyo na maana.

Wanachama wa CCM wakiwa na Ndugu Polepole

Polepole ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na mamia ya Vijana wa CCM mkoani Mwanza katika uzinduzi wa kampeni ya "Nyamagana ya Kijani" uliofanyika Juni 16, 2019.

''Nasisitiza viongozi wanaokiuka misingi ya maadili ya CCM, Chama hakitasita kuwachukulia hatua viongozi wenyewe au vikao ambavyo vitakwenda kinyume na misingi ya CCM'', ameeleza Polepole.

Aidha Ndugu Polepole ametolea mfano vikao hivyo kuwa ni kama vile vitakavyoweka msimamo wa kumbeba mwanachama mgombea na kwamba vikao hivyo vitachukuliwa hatua pia ili kulinda nidhamu ya chama.

Pia amewaeleza vijana wa CCM kuwa wao ni ngao ya viongozi wa CCM, hivyo waendelee kumlinda, kumtetea na Kumuunga Mkono Ndugu John Pombe Joseph Magufuli, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania na kuwapinga viongozi wanaotaka kumuangusha kwa hila na wasiofuata utaratibu kupitia vikao.