Jumatano , 17th Feb , 2021

Wananchi wa Kijiji cha Njinjo, kata ya Njinjo wilayani Kilwa mkoani Lindi, wameiomba serikali kuwasaidia ujenzi wa shule yao mpya ambayo wanafunzi wake wanasomea chini ya miti baada ya shule yao ya zamani kusombwa na mafuriko Januari 25, 2020.

Wanafunzi wa shule ya msingi Njinjo, wakiwa chini ya mti

Hayo wameyaeleza baada ya kusimamisha msafara wa Naibu Waziri wa TAMISEMI David Silinde, aliyekuwa anapita njia kutoka Kilwa Kivinje kukagua miradi mbalimbali ya serikali akielekea Liwale na kumuomba aone jinsi wanafunzi hao wanavyosoma chini ya miti.

Aidha wananchi hao wamesema kuwa mpaka sasa wamejitahidi kujenga madarasa matatu ambayo tayari wamekamilisha kuyajenga kwa nguvu zao pamoja na fedha milioni 30 kutoka halmashauri ya wilaya ya Kilwa na sasa wamepokea milioni 64 kutoka TAMISEMI ambayo wameambiwa wajenge madarasa matano na sasa wapo katika hatua ya uchimbaji wa msingi na kufyatua matofali.