Jumanne , 15th Oct , 2019

Hali ya sintofahamu na majibizano ya maneno imeibuka mkoani Kigoma, baina ya Maafisa wa Serikali na wananchi wa Kijiji cha Kaseke kilichopo wilayani Kigoma mkoani humo, juu ya uhalali wa kuandikishwa kwa vijana wa mafunzo ya JKT kwenye daftari la kupiga kura.

Kwa mujibu wa wanakijiji hao wamedai kupinga kuruhusiwa kwa vijana wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa JKT kikosi cha 821 KJ Bulombora, kujiandikisha katika daftari la wapiga kura katika kijiji chao kwa kile walichokieleza ni tofauti na miaka iliyopita.

Hali hiyo imetokea wakati Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma, Rashid Mchata, pamoja na Maafisa wengine wa Serikali walipokuwa katika ziara ya kuangalia namna zoezi la uandikishaji linavyoendelea, ambapo wananchi wamehoji kuwa hawajawahi kuona wazalendo hao wakipiga kura Serikali za Mitaa.

Wananchi hao wameeleza kuwa vijana wa JKT mara kwa mara, wamekuwa wakishiriki kwenye chaguzi za Serikali Kuu tu, na huwa hawaruhusiwi kupiga kampeni jeshini.

Zoezi la uandikishaji wa wananchi kwenye daftari la wapiga kura kueleka uchaguzi wa Serikali za Mitaa linatarajiwa kufungwa Oktoba 17, 2019, baada ya kuongezwa siku 3 na Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo.