Jumatatu , 16th Jul , 2018

Kikundi cha watu wapatao 100 wenye hasira kali nchini Indonesia kimeua mamba takribani 300 baada ya mamba mmoja kujeruhi na kumuua mfugaji aliyekuwa akitafuta malisho.

Mamba waliouwawa na wananchi nchini indonesia

Tukio hilo limetokea katika jimbo la Papua ambapo, Sagito (48) alitumbukia katika bwawa linalotunza mamba hao wakati akitafuta majani ya kulisha mifugo yake.

Kikundi hicho cha watu pamoja na majirani walikasirishwa na uwepo wa bwawa hilo karibu na makazi ya watu ndipo walipoelekea kituo cha Polisi kutoa taarifa lakini licha ya mmiliki wa bwawa kukubali kulipa fidia, wananchi hao hawakukubaliana na uamuzi na kuamua kuwauwa mamba hao.

Mamlaka ya Polisi nchini humo imekiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba ipo katika uchunguzi baada ya kukamilika itafungua mashitaka kwa wahusika wa mauwaji hayo.

Matukio ya mamba kuuwa raia yanakithiri nchini humo, mwezi Machi maafisa wa wanyama walifanikiwa kumuuwa kwa risasi mamba mwenye urefu wa mita sita ambaye alimla mfanyakazi mmoja wa shamba la michikichi.

Miaka miwili iliyopita pia mtalii mmoja raia wa Urusi alivamiwa na mamba katika kisiwa maarufu cha watalii kuogelea cha Raja Ampat nchini humo.