Jumapili , 23rd Sep , 2018

Waziri wa Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema hadi mazishi ya kitaifa yanafanyika, jumla ya watu 224 walikuwa wamepoteza maisha kutokana na ajali ya kivuko cha MV. Nyerere kilichotokea Septemba 20, mwaka huu, huku idadi kubwa waliyofariki ikiwa ni wanawake.

Waziri wa Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe

Waziri Kamwelwe amebainisha hayo wakati akitoa taarifa ya tukio zima mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye ameongoza mazishi na amesema kuwa wanawake waliopoteza maisha jumla yao ni 126, wanaume 71, watoto wa kike ni 17 na wa kiume ni 10.

Aidha, Waziri Kamwelwe amesema ajali hiyo ilitokea Septemba 20,2018 majira ya saa 7:48 mchana na taarifa zilifikishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza saa 8:10 mchana ambapo yeye na Kamati ya Ulinzi ya Usalama ya Mkoa walikimbia kuwahi eneo la tukio na kukuta watu watu 40 wameshaokolewa na wakazi wa kisiwa cha Ukara.

Awali, kabla ya ibada kuanza, idadi ya waliopoteza maisha ilikuwa 223 lakini mwili mmoja wa mwanamke ulipatikana mchana wa leo na kufanya idadi yao kufikia 224.

"Mipango ya serikali ya muda mrefu ni kujenga kivuko kikubwa ambacho kitakuwa kikifanya safari zake kati ya bandari ndogo ya Bugolora iliyopo kisiwa cha Ukerewe na kisiwa kidogo cha Ukara. Tumefanya utafiti kwenye visiwa vidogo vyote na kubaini kuna mialo zaidi ya 140. Hii itaimarishwa ili iweze kufikika na vyombo vya usafiri ambavyo ni imara", amesema Waziri Kamwelwe.

Kwa upande wake, Mbunge wa Ukerewe Joseph Mkundi ambaye ni mzaliwa wa kisiwa cha Ukara, amesema wilaya ya Ukerewe inahitaji kupatiwa usafiri wa uhakika baina yake na visiwa jirani ili kuepuka maafa kama hayo yasitokee.

"Ukerewe tunahitaji chombo kizuri cha uhakika kinachoweza kustahimili maafa kama haya yasitokee. Ni kipindi kigumu kwetu wana Ukara, niombe tushikamane", amesema Mkundi.

 Ajali ya kivuko cha MV. Nyerere kilichozama Septemba 20, 2018 kimesababisha takribani watu 224 kufariki ambao kwa sasa wamezikwa katika makaburi ya pamoja yaliyopo viwanja vya shule ya sekondari ya Bwisya mita 250 kutoka gati la Bwisya.

Hadi sasa serikali imeshaanza kuchukua hatua madhubuti ya kukitoa kivuko hicho majini kwa kutumia burudoza lililowasili katika kisiwa cha Ukara, wilayani Ukerewe na limeanza zoezi la kuvuta kivuko hicho katika Ziwa Victoria, na kukipeleka nchi kavu ambapo zoezi hilo linatarajiwa kukamilika kwa muda wa wiki moja tokea sasa.