Jumapili , 20th Sep , 2020

Katika Kusherekea siku ya usafi duniani leo Septemba 20,2020 wananchi mkoani Geita wamejitokeza maeneo mbalimbali ikiwemo katika vituo vya mabasi, taasisi za Elimu na barabara za mitaani kwa ajili ya kujitolea kufanya usafi huku wakitahadharishwa kuepuka kuharibu mazingira.

Wakazi wa Geita wakifanya usafi

Afisa mazingira wa halmashauri ya mji wa Geita, Albert Auson amesema kuwa  mwananchi yeyote  atakayeenda kinyume na hapo  ataadhibiwa  kwa kufuata sheria ya usafi na mazingira ambapo atakayekamatwa atalipa faini kuanzia laki mbili hadi milioni moja au kwenda jela miezi 24 au vyote kwa pamoja.

Kwa upande wa wakazi wa mkoa huo wamesema kuwa wameamua kufanya hivyo ili kupunguza magonjwa ya mlipuko ambapo  pia wamewatahadharisha wale wote ambao watakuwa wachafuzi wa mazingira kuwa sheria itachukua  mkondo wake.

"Wengi wametelekeza  maeneo kama haya ya hifadhi ya barabara na kuiachia manispaa ifenye usafi jambo ambalo si sahii mana hata manispaa kuna baadhi ya maeneo wanashindwa kufika,kila raia ambaye amezungukwa na maeneo ambayo ni machafu anapaswa kusafisha kwani mazingira ukiyatunza na yenyewe  yanakutunza’’, amesema Jonathan James.