Watekwaji waambiwa waseme ukweli

Alhamisi , 11th Jul , 2019

Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu hapa nchini (THRDC), umetoa rai kwa wale wahanga wote wa utekwaji, wanapotoka hadharani na kuongea na umma waeleze kinagaubaga kilichowakuta, ili kuondoa sintofahamu miongoni mwa watu wengi.

Mratibu wa THRDC Onesmo Olengurumwa

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Mtandao huo Onesmo Olengurumwa, wakati akitoa tamko la kuhusu matukio ya upoteaji na utekwaji, na kutoonekana kwa watu yanayoendelea hapa nchini, ambapo amesema matukio haya yanaleta taswira mbaya ndani na hata nje ya nchi.

''Inaweza ikawa inachangia na kuwapa wale watu, wanaofanya utekaji nguvu zaidi, kwamba tunaowateka hata tukiwaachia hawaendi kusema chochote, tuanawasihi sana mnapopata fursa ya kurudi ni vyema ukaongea yale yote yaliyokusibu, na kuweza kuwapa moyo na nguvu watu ya kupiga kelele'', amesema.

Aidha Olengurumwa, ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wabunge wake waingilie kati suala hili, na wao walisimamie ili mwisho wa siku waje na maadhimio ya kuona ni namna gani suala hili litaisha.