Ijumaa , 15th Mar , 2019

Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Mh. Joachim Wangabo ametoa siku saba kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, kuhakikisha anaunda timu ya uchunguzi ili kuwabaini wadaiwa wa shilingi bilioni 1.34 za makusanyo ya mapato.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mh. Joachim Wangabo

Amesema hayo baada ya kupitia taarifa za makusanyo na kubaini tatizo la kutowasilishwa kwa makusanyo ya mapato ya ndani kwa kutumia mfumo wa Local Governent Revenue Collection Information System (LGRCIS) na kueleza kuwa kumekuwa na watendaji ambao sio waaminifu wanaokabidhiwa makusanyo hayo  na kuyaingiza kwenye matumizi binafsi.

Amesema watumishi hao huzitumia pesa hizo katika biashara zao wakitegemea kurudisha na matokeo yake bili za wakusanyaji hazikubali kutoka kwenye mfumo hadi fedha zote alizokusanya zitimie.

Akitolea mfano Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Mh. Wangabo amesema kuwa, “hadi kufikia mwezi Februari mwaka 2019, jumla ya Shilingi Milioni 98 zimetumika kama sehemu ya gharama za wakusanyaji baada ya kuzikata na kutumia. Matokeo yake fedha zinapelekwa halmashauri zikiwa pungufu na kuongeza kuwa jumla ya shilingi 241 za halmashauri hiyo zilitumika kabla ya kupelekwa benki jambo hilo ni kinyume na kifungu cha 32 cha Memoranda ya Fedha za Serikali za Mitaa”.

Alitoa agizo hilo wakati wa ufunguzi wa semina ya mafunzo elekezi kwa waheshimiwa madiwani kutoka katika halmashauri zote nne za Mkoa wa Rukwa iliyofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Sumbawanga ambapo Mh. Wangabo alikuwa mgeni rasmi wa semina hiyo.  

Akitoa neno la Shukurani kwa mgeni rasmi mstahiki Meya wa manispaa ya Sumbawanga alipongeza juhudi za mkuu wa mkoa wa Rukwa kuhakikisha anasimamia vyema maendeleo ya mkoa huo, na kumuhakikishia kuwa hawatamuangusha katika kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unaongezeka.

Hadi kufikia tarehe 12 mwezi Machi mwaka 2019, Manispaa ya Sumbawanga ina wadaiwa wa makusanyo ya mapato ya ndani shilingi milioni 45.97, Sumbawanga Vijiji Shilingi Milioni 756.17, Wilaya ya Kalambo Shilingi Milioni 252.64 na Wilaya ya Nkasi Shilingi Milioni 290.95.

Bonyeza hapa chini kutazama zaidi.