Jumatano , 14th Aug , 2019

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Astashata Nditiye amesema serikali inalishughulikia suala la makato makubwa kwa watumiaji wa mitandao ya simu kutokana na malalamiko mengi yaliyoripotiwa.

Nditiye ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye kipindi cha East Africa Breakfast kuhusiana na malalamiko ya wananchi kupanda kwa gharama za simu na kusema kuwa yeye ni miongoni mwa wahanga wa kukatwa gharama kubwa za matumizi ya simu.

Nditiye amesema kuwa, "ni kweli kuna malalamiko kwa wananchi kuhusu gharama za simu zimekuwa kubwa, wakati mwingine wakiweka pesa inakatwa hata kama hajaongea".

"Hata kwangu mimi nilishawahi kujiunga bando la saa moja, nikawa naongea ilipofika dakika 43, nikaambiwa bando la kuzungumza limeisha, kwa hiyo kama Serikali tumelipokea." amesema Nditiye

Kuhusiana na matumizi ya simu Tanzania,  Nditiye amesema kwa sasa kuna watumiaji wa simu milioni 40, ambapo ni sawa na asilimia 94 ya Watanzania wote.