Jumapili , 8th Dec , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inatarajia kufungua kitengo cha Tiba za Mifupa na Misuli katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara Kwangwa Mara hospitali hiyo itakapokamilika kujengwa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa Hospitali hiyo iliyopo Manispaa ya Musoma mkoani Mara, Waziri Mkuu amesema kitengo hicho kitakuwa cha pili kwa ukubwa kikifuatia cha MOI Muhimbili.
 
Lengo la kufungua kitengo hiki kwenye hospitali hii ni kusogeza huduma karibu na wananchi hususani wa Kanda ya Ziwa ambao kwa sasa wanategemea huduma hizo kutoka Hospitali ya Bugando, jijini Mwanza ambayo pia imezidiwa kutokana na udogo wa kitengo hicho kwenye hospitali hiyo,” amesema.

Amesema kuwa ujenzi wa Hospitali ya Kwangwa ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano ambapo mbali na kutoa huduma za afya lakini pia hospitali hiyo itafungua fursa zaidi za kiuchumi kwa mkoa wa Mara.

Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliagiza kutolewa kwa shilingi bilioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo uliokwama kwa zaidi ya miaka 40 na ameridhishwa na ujenzi wake unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Bw. Adam Malima alisema hospitali hiyo inatarajiwa kuanza kutoa huduma ya mama na mtoto ifikapo Februari, mwakani baada ya kukamilika kwa jengo A (wing A) mapema mwakani.