Jumatano , 17th Apr , 2019

Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda, amedai wizara yake ina udhaifu mkubwa katika baadhi ya maeneo ikiwemo kushindwa kusimamia utekelezaji wa sera ya viwanda, kwa kukosa wataalamu wa sera ya viwanda kwenye ngazi za Mikoa na Halmashauri.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda.

Waziri Kakunda ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema ukosefu wa maofisa wa viwanda mikoani na kwenye Halmashauri kumeleta udhaifu kwenye upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu usajili wa viwanda.

"Napenda nikiri wizara yangu ina udhaifu mkubwa katika kusimamia utekelezaji wa sera zilizo chini ya uratibu wake, ni vizuri utaratibu wa utekelezaji wa majukumu ikiwamo takwimu za viwanda uanzie kwenye halmashauri."

Ikumbukwe kuwa Matumizi ya msamiati 'dhaifu' umepelekea mvutano wa maneno baina ya Spika wa Bunge na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali nchini, CAG Profesa Assad baada ya kutoa kauli hiyo akiwa nje ya nchi na kupelekea kuitwa kwenye kikao cha kamati ya maadili ya Bunge. Ripoti kutoka katika kikao hicho iliazimia kutofanya kazi na CAG huku mwenyewe akisisitiza kuendelea kulitumia neno hilo.

Aprili 14, 2019 Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai alimtaka CAG kujitafakari kwenda kujieleza kwa Rais baada ya Bunge kufikia maamuzi dhidi yake.