Jumanne , 5th Mar , 2019

Baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof Palamagamba Kabudi kuwataka Watanzania kuwa wazalendo na nchi yao na kutoisema vibaya au kuidhihaki, amekosolewa na makundi mbalimbali ya kijamii wakisema serikali itaendelea kusemwa vibaya na siyo nchi.

Waziri wa Mambo ya Nje, Prof. Kabudi

Baada ya kauli hiyo, mjadala mzito umezuka kwa viongozi na watu mbalimbali katika mtandao wa Twitter wakidai kwamba katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali haijatajwa kama ni nchi.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amesema kwamba yeye ataendele kusema mabaya ya serikali ya nchi yake popote na wakati wowote.

"Ninaipenda sana nchi yangu Tanzania. Nimeitumikia kwa weledi kila nipatapo nafasi ya kufanya hivyo. Nimeilinda nchi yangu dhidi ya majaribu mbali mbali. Nitaisema vibaya Serikali ya Nchi yangu popote na wakati wowote inapofanya Mambo kinyume ya misingi ya katiba ya Tanzania," Zitto Kabwe.

Rapa wa muziki wa Bongo Fleva, Webiro Wasira "Wakazi' amesema kwamba Wanaoisema nchi siyo watanzania lakini kwa upande wake atazidi kuikosoa serikali pale inapoenda tofauti.

"Professor PK anafahamu hili, na inathibitishwa kwa matamshi yake na msisitizo wake. Anajaribu sana, maskini. Wanaoweza kuisema nchi yetu sio sisi, labda ungewa address kwa English. Ila mimi nitaendelea kuisema Serikali ikizingua kama kawaida," Wakazi.

Mwanasheria Jebra Kambole amesema kwamba,  "tofautisha nchi na serikali!! Nchi hatutaisema vibaya maana nchi ni wananchi, tutaitetea Daima!!! Lakini tutaisema na kuibagaza kadili Mungu atakavyotupa uhai!!!. Yani tutaibagaza serikali aseeeeeee!".

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amesema kwamba  Profesa Kabudi  ajulishwe kwamba hawatanyamazishwa na uovu wao, au vitisho vyao, au  ulaghai na propaganda zao, au na hongo na rushwa zao.

"Mwambieni Profesa Kabudi kwamba tutaendelea kuyasema hadharani, popote pale, ndani na nje ya Tanzania, maovu ya Serikali yetu, na ya vyombo vyake, na ya viongozi wake na ya watendaji wake", amesema Lissu.