Waziri Majaliwa, hali ya sasa ya Corona nchini

Jumapili , 24th Mei , 2020

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa mpaka sasa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ujumla wake, umebaki na wagonjwa wa Virusi vya Corona 13, Kibaha wamebaki wagonjwa 16 na Mkoani Dodoma katika kituo cha Mkonze wamebaki wagonjwa 3.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu ameyabainisha hayo leo Mei 24, 2020, wakati akizungumza na waumini wa Dini ya Kiislam mara baada ya kumaliza kuswali Sala ya Eid El Fitri katika Msikiti wa Gaddafi, jijini Dodoma. 

"Nafurahi kuwaambia kuwa taarifa ya Daktari Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, leo asubuhi Hospitali ya Amana imebaki na mgonjwa mmoja, Mloganzila amebaki mmoja, Temeke hatuna mgonjwa wa Corona, Kairuki, Rabininsia na Regency hakuna mgonjwa, katika Hospitali ya AgaKhan tunao 11, 4 wako chini ya uangalizi wa Daktari, Kibaha wamebaki 16, na Dodoma katika Kituo cha Mkonze wamebaki watatu" amesema Waziri Mkuu.

Aidha Waziri Mkuu ametoa salamu kutoka kwa Rais Magufuli, ambapo amewapongeza Waislam kote nchini kwa kumaliza mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani na amewashukuru kwa namna walivyoshiriki kuliombea Taifa, hasa katika kipindi hiki cha ugonjwa wa COVID-19.