Jumatatu , 16th Jul , 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule awakamate viongozi wa Chama cha Msingi cha Mkombozi kwa upotevu wa dola za Kimarekani elfu 21 za chama hicho sawa na takribani milioni 47.8 za kitanzania.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Julai 16, 2018 wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa kijiji cha Kangeme, kata ya Ulowa katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama ambapo alienda kuzindua mpango wa Ushirika Afya na
NHIF.

"Wabebe hawa watu, wahoji waseme hiyo fedha iko wapi na jambo la kwanza wailete hiyo fedha ya wakulima. wakishindwa kurejesha fedha, wawekwe ndani",amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu amefikia uamuzi huo baada ya kuwaita viongozi wa chama cha Mkombozi watoke hadharani na kubaini kuwa hakuwepo hata mmoja. huku ikidaiwa kwamba walitoroka baada ya wananchi kuanza kuzomea.

Kwa upande wake, Kamanda Haule amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Mwenyekiti, Bw. Shilinde Abdallah na mhasibu wa AMCOS hiyo, Bw. Kulwa Shinzi pamoja na wajumbe saba wa bodi ya chama hicho.