Jumapili , 5th Jul , 2020

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Kampuni ya Xiamen Ongoing Construction Group inayojenga  Bandari ya Karema kwa gharama za zaidi ya sh. bilioni 47 ifanye kazi usiku na mchana na  kukamilisha ujenzi huo kwa wakati ili kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Congo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Pia, Waziri Mkuu ametoa muda wa siku 21 kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Polisi, Wizara ya Madini na wawe wameanza kutoa huduma katika eneo la Ikola ili kuhudumia wageni wanaotoka Congo.

Alitoa agizo hilo baada ya kuweka jiwe la msingi la  ujenzi wa Bandari ya Karema inayojengwa kwenye ziwa Tanganyika katika kata ya Karema wilayani Tanganyika, Katavi. Alisema mkandarasi anatakiwa ahakikishe mradi huo unakamilika haraka.

“Tumeamua kujenga bandari hii ambayo itawezesha meli zaidi ya moja kupakia na kushusha abiria na mizigo kwa wakati mmoja. Hii ni Serikali ya kuahidi na kutekeleza na ni Serikali ya kusikia na kutenda na ndio maana halisi ya falsafa ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi Tu.”

Waziri Mkuu alisema mradi huo unalenga kuongeza tija katika shughuli za kibandari kwenye ukanda wa Ziwa Tanganyika ndani na nje ya nchi na kwamba utaongeza fursa za kibiashara nchini na pia utakuwa chachu ya kukuza uchumi pamoja na kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi.