Jumatano , 18th Jul , 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameonyesha kushangazwa na mila na tamaduni ya kucharazana bakora kwenye jamii ya washirazi katika kijiji cha Mwaka Kogwa, Makunduchi Kusini visiwani Unguja, Zanzibar.

Wananchi wa Mwaka Kogwa wakisherehekea sherehe hiyo

Mapigano hayo yaliyodumu kwa masaa matatu yalishuhudiwa wananchi ambao walipigana kwa fimbo za majani ya migomba kama ishara ya mila na tamaduni za kijiji chao.

Akizungumza baada ya kushuhudia sherehe hiyo, Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa amepigwa na mshangao mkubwa kuona namna ambavyo wananchi hao wanavyopigana huku wakiwa na furaha.

"Ni kweli sijapata kuona namna ambavyo watu wanachapana viboko namna hii huku wakiwa na furaha, hii ni mara yangu ya kwanza kuona ", amesema  Majaliwa.

Amesema utamaduni kama huo unajenga msingi mzuri wa maisha na kusisitiza kuwa kuduumisha kwake ni kuvirithisha vizazi vijavyo.

Wananchi wa Mwaka Kogwa wakisherehekea sherehe hiyo.

Waziri mkuu Majaliwa pia amesema utamaduni ni fursa nzuri ya kiuchumi hasa ikizingatiwa kuwa sherehe hizo zinahudhuriwa na watalii kutoka sehemu mbalimbali Duniani.

Sherehe hizo hufanyika kila mwaka katikati ya mwezi Julai na Agosti, ikiwa inahusisha kuimba nyimbo na kucheza ngoma zinazoashiria kutakiana mafanikio mema miongoni mwa watu wa jamii hiyo katika mwaka husika.