Jumatatu , 11th Nov , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Novemba 3, 2019, Serikali imeshatoa mikopo ya Sh. Bilioni 162.8 kwa wanafunzi 46,838 wa mwaka wa kwanza nchini kote.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

“Kwa mwaka 2019/2020, Serikali imetenga jumla ya shilingi Bilioni 450 kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi walengwa 128,285. Na hadi tarehe 3 Novemba, 2019 wanafunzi 46,838 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka 2019/2020, walikuwa wamepewa mikopo inayofikia shilingi bilioni 162.8,” amesema.

Ametoa kauli hiyo Novemba 10, 2019, wakati akizungumza na maelfu ya waumini waliohudhuria Baraza la Maulid kitaifa, katika viwanja vya Benki Kuu (BoT) Capripoint, jijini Mwanza.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli, alisema Serikali inatambua kuwa utoaji wa huduma ya elimu ni gharama na kuwa baadhi ya wananchi hawawezi kumudu gharama hizo, hivyo ikaamua kuanzisha utaratibu wa kutoa mikopo ya elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.

“Mikopo inayotolewa na Serikali, huongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (Sura 178) inayotaja vigezo vya wahitaji na wenye udahili lakini wasio na uwezo wa kumudu gharama zote au sehemu ya gharama za mafunzo au kwenye maeneo ya kipaumbele ikiwemo yatima na wanaotoka familia zenye kipato duni.”