Waziri Mkuu atoa agizo kuhusu maeneo ya michezo

Jumatatu , 10th Jun , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameagiza halmashauri zote za majiji na miji, zihakikishe kuwa kuanzia sasa zinatenga maeneo ya michezo na burudani kila zinapopima viwanja.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Jumatatu, Juni 10, 2019, wakati akifungua mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa shule za msingi na sekondari Tanzania, katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara ambapo zaidi ya wanafunzi 5,400 wanashiriki mashindano hayo.

“Naagiza kuanzia sasa, maeneo yote yanayopimwa na halmashauri na miji yote nchini, lazima yazingatie uwepo wa maeneo ya michezo na burudani,” amesisitiza Waziri Mkuu.

Pia, amezitaka Halmashauri ziweke mpango madhubuti wa kuyaendeleza maeneo ya michezo na burudani sambamba na miundombinu inayozingatia mahitaji ya wote bila kubagua.

Amesema katika baadhi ya maeneo kumekuwepo na uhaba wa viwanja vya michezo kwa sababu ya mipango miji isiyozingatia mipango endelevu ya sekta mbalimbali.

Hivyo, Waziri Mkuu ameagiza yafanyike marekebisho na hatua za haraka ili kutoa fursa ya ukuaji wa michezo na kusaidia wananchi kushiriki michezo, mazoezi na kupata burudani.

Amesema ifikapo Septemba 30, 2019, kila halmashauri iwe imefanya mapitio ya maeneo yote yaliyokuwa yamepimwa kwa matumizi ya huduma maalum ikiwemo michezo, burudani, shule na ibada na kutoa taarifa kama yanatumika kwa ajili hiyo au vinginevyo.