Alhamisi , 17th Oct , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama na Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda ya Kusini, wafike ofisini kwake Dar es Salaam kesho asubuhi na taarifa kuhusu skimu wa umwagiliaji wa Narunyu.

Kassim Majaliwa

Ametoa agizo hilo leo Alhamisi, Oktoba 17, 2019, wakati alipoenda kukagua skimu hiyo ambayo imekuwa ikilalamikiwa tangu 2017. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mtama ni Bw. Warioba Gunze na Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda ya Kusini, ni Mhandisi Mndeme.

Amechukua uamuzi huo baada ya kufika eneo la mradi na kupokea malalamiko ya wanajumuiya ya umwagiliaji kutoka kwa Mwenyekiti wao, Bw. Bakari Awadhi juu ya kusuasua kwa mradi huo lakini alipotaka apate maelezo ya wataalamu hakuna hata mmoja ambaye alikuwepo.

"Nilitaraji niwakute hapa Mkurugenzi wa Halmashauri, Afisa Umwagiliaji wa Wilaya na Mkurugenzi wa Umwagiliaji wa Kanda. Nimeagiza wanikute uwanja wa ndege Lindi au Dar es Salaam na kesho asubuhi waje ofisini kwangu wanipe taarifa kamili ya mradi huu. Nataka nijue fedha zilizobakia zaidi ya sh. milioni 240 ziko wapi."

"Walipaswa niwakute hapa wananisubiri kwa sababu nilitoa taarifa tangu jana kwamba nitapita hapa. Nimepata taarifa kwamba wamesafiri kutoka Mtwara na leo asubuhi walikuwepo Lindi mjini. Waje ofisini kesho, wakishindwa, nitachukua maamuzi mengine," amesema.

Akielezea umuhimu wa mradi huo wakati akizungumza na baadhi ya wanaushirika waliokuwepo, Waziri Mkuu amesema ni wa muhimu kwa sababu unatiririsha maji wakati wote. "Huu ni mradi wa kuringia. Mradi huu unatiririsha maji wakati huu wa kiangazi, tena mengi tu."