Waziri Mkuu wa Burundi arejea nyumbani

Jumatano , 29th Jul , 2020

Waziri Mkuu wa Burundi Jenerali Alain Guillaume, leo amerejea nchini kwake hii ni baada ya hapo jana kumwakilisha Rais wa nchi hiyo Evarist Ndayishimiye, kwenye shughuli ya Kitaifa ya kuuaga mwili wa Rais Mstaafu Hayati Benjamin Mkapa, kwenye Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, akiagana na Waziri Mkuu wa Burundi Jenerali Alain Guillaume.

Katiba hotuba yake hapo jana Julai 28, Waziri Mkuu huyo alitoa salamu za pole na rambirambi kwa Rais Magufuli kutoka kwa Rais wake pamoja na Warundi kiujumla.

"Warundi wanawapa pole, wanawafariji, Mh Rais, Rais wangu amenituma upokee salamu kutoka kwake, anakufariji kwa matatizo makuu na msiba mkuu ulioweza kuipata Tanzania na Burundi, sitozungumza marefu kwa nyakati kama hizi", alisema Jenerali Guillaume.

Waziri Mkuu huyo wa Burundi amesindikizwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa.

Rais wa Awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa, alifariki Dunia usiku wa kuamkia Julai 24, 2020, na atazikwa leo Julai 29, 2020, Kijijini kwao Lupaso, Masasi mkoani Mtwara.