Waziri wa Ulinzi atangaza kujiuzulu

Jumamosi , 13th Apr , 2019

Waziri wa Ulinzi nchini Sudan Awad Ibn Aouf ametangaza kujiuzulu kwenye nafasi yake ya uongoi wa Serikali ya Mpito, ikiwa ni siku chache baada ya Jeshi nchini humo kutangaza kumuondoa Rais Omar al-Bashir ambaye aliiongoza nchi hiyo kwa miaka 30.

Waziri wa Ulinzi nchini Sudan Awad Ibn Aouf

Awad Ibn Aouf taarifa zake zimeanza kusambaa mapema leo asubuhi ambapo zimezua taharuki maeneo mbalimbali nchini humo kutokana na kiongozi huyo hivi karibuni kuonekana kwenye vyombo vya habari akitangaza kuondoa utawala wa Rais Al-Bashir.

Jenerali Awad Ibn Ouf alitangaza kuunda Serikali ya mpito baada ya kuongezeka kwa maandamano ya raia wa Sudan ambao walionekana kuukataa utawala wa Rais Bashir kwa kufanya maandamano.

Uamuzi wa Jenerali Awad Ibn Ouf umezua sintofahamu miongoni mwa wachambuzi wa siasa Afrika wakihoji huenda uamuzi huo ukawa shinikizo la baadhi ya Wanajeshi wenzake kufuatia kiongozi huyo kuwa mshiriki wa Al-Bashir kwa muda mrefu.

Alhamis ya wiki hii Gen Ibn Auf akiungana na Wanajeshi  wenzake kufikia maamuzi ya kumuondoa Rais Al-Bashir kufuatia maandamano yasiyokuwa na kikomo yaliyokuwa yakifanywa na wananchi.