Jumamosi , 21st Jul , 2018

Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Charles Mwijage ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Frank Kanyusi ambaye anakuwa mkurugenzi wa pili kutenguliwa wiki hii.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Jenister Mhagama (kulia) na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Charles Mwijage.

Kutenguliwa kwa Kanyusi kumetokea siku moja tu baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Jenister Mhagama, kutengua uteuzi wa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Ajira nchini (TaESA), Saneslaus Chandarua.

Ingawa taarifa ya kutenguliwa mkuu huyo wa BRELA haikutaja sababu, taarifa ya Mhagama juzi imetaja sababu nne za kumtengua kaimu mtendaji mkuu wa TaESA, ambapo Waziri ametaja sababu hizo kuwa ni pamoja na kushindwa kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri pamoja na upatikanaji wa ajira.

Utenguzi wa Mkurugenzi huyo  wa BRELA ulianza jana Julai 20, 2018 ambapo taarifa imesema kuwa atapangiwa kazi nyingine.

Kwa Upande wa Waziri Mhagama sababu za kumtengua  mtendaji mkuu wa TaESA ni pamoja na kushindwa kuunganisha watafuta kazi na waajiri, kuratibu na kuwezesha upatikanaji wa ajira ndani na nje ya nchi, kukusanya, kufanya uchambuzi na kusambaza taarifa za soko la ajira kwa wadau na umma kwa ujumla.

Mkurugenzi huyo aliteuliwa mwaka 2014 baada ya aliyekuwa Mkurugenzi wa BRELA kustaafu, hivyo amedumu kwenye nafasi hiyo kwa muda wa miaka minne.