Alhamisi , 11th Oct , 2018

UPDATE: Saa 1:00 Usiku,
Kamanda wa Polisi kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema watu wanaoshikiliwa kwaajili ya mahojiano kutokana na tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji 'MO Dewji' wamefikia 12.

Mfanyabiashara Mo Dewij.

Akizungumza na www.eatv.tv, Mambosasa amesema kuwa hadi sasa watu 12 wameshikiliwa ili kusaidia uchunguzi wa tukio hilo lililotokea mapema leo alfajiri, kati ya hao waliokamatwa ni pamoja na walinzi wa hoteli ya Collesium, mahali ambapo tukio hilo limetokea.

"Kwa sasa wako 12 wakiwamo walinzi wote watano wa Kampuni ya G1 inayosimamia ulinzi wa hoteli hiyo, pia kuna security Manager (afisa usalama) wa hoteli," amesema Mambosasa
 

UPDATE: Saa 10:50 Asubuhi 

“Haiwezekani mahali hapa watu wakaingia kirahisi namna hii, cctv camera haionyeshi vizuri upande walioingilia, kwa hiyo pengine yalikuwa ni maandalizi ya kuweka mazingira hivyo, lakini pia walipiga risasi juu na kumteka kumuingiza kwenye gari, kitendo hicho sio chepesi hakuna filimbi iliyopigwa, hakuna mayowe mpaka taarifa tunakuja kuipata baadaye kiasi hicho”. - Kamanda wa Polisi Kanda maalum Dar es salaam Lazaro Mambosasa.

UPDATE: Saa 10:45 Asubuhi 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amekanusha taarifa za kupatikana kwa mfanyabishara Mohammed Dewji, na kwamba taarifa zilizosambaa kuwa amepatikana sio sahihi.

"Jambo hili sio la kisiasa, wanasiasa wasitumie ajenda hii kujipatia umaarufu, watumie jambo hili kama kulinda amani na utulivu wa mkoa wetu". - Mkuu wa Mkoa wa Da es salaam Paul Makonda. 

UPDATE: Saa 9:24 asubuhi

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Lazaro Mambosasa amesema kwamba wameweka vizuizi kuhakikisha hakuna mtu anayetoka, ili watekaji wasitoke nje ya nchi, na kwamba waliohusika kwenye tukio la kumteka Mo Dewij ni raia wawili wa kigeni (wazungu).

Mambosasa amesema kuwa tayari wameweka vizuizi kuhakikisha hakuna anayetoka, ili watekaji wasitoke nje ya nchi.

Tukio hilo limetokea katika ‘Gym’ ya Colosseum iliyopo Oysterbay jijini Dar es salaam ambapo mfanyabiashara huyo alipokuwa akiingia kufanya mazoezi.

Akizungumza na www.eatv.tv leo asubuhi Oktoba 11, 2018, Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kinondoni, Jumanne Murilo amesema baada ya kupata taarifa za tukio hilo wanafuatilia kujua ukweli wake.

Gari ya mfanyabishara Mo Dewij ikiwa eneo la hoteli ya Collesium ambalo alitumia kufika eneo la Gym.

Saa 2:00 Asubuhi

Mfanyabishara maarufu nchini ambaye pia ni muwekezaji wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji (MO) amedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana, saa 11 Alfajiri ya leo.

Kamanda wa Polisi wa kanda maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa ametoa taarifa za awali kwa waliohusika katika utekaji wa mfanyabiashara maarufu Mo Dewji kuwa ni watu wawili ambao ni raia wa kigeni.

Dereva wa Uber (jina linahifadhiwa) amesema aliona  watu wakishuka kwenye gari dogo, hoteli ya Collessium wakiwa wamejifunika usoni, wakapiga risasi moja juu na kumchukua Mfanyabiashara maarufu nchini Mohammed Dewji 'Mo'

Dewji ni mwekezaji wa klabu ya Simba akiwa na hisa 49 na amekuwa akiingia katika chati ya juu ya jarida la Forbes kama miongoni mwa matajiri vijana Afrika.

Kwa upande wake baba mzazi wa Mo Dewij amesema kuwa taarifa za kutekwa mwanae zimempa mshtuko na anatumaini Jeshi la Polisi litafanya kazi yake kwa ufanisi zaidi.

Endelea kufuatilia EATV, EA Radio na www.eatv.tv kwa taarifa zaidi.