Jumatano , 21st Feb , 2018

Madiwani wawili wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoka kata za Terati na Daraja mbili katika Jiji la Arusha wamejiuzulu nyadhifa zao na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Madiwani hao ni pamoja na Prosper Msofe (Daraja mbili na Obeid Meng'oriki (Terati) ambao kwa pamoja wameamua kujiunga na CCM ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Dkt. John Magufuli.

Msofe ambaye aliwahi kuwa Naibu Meya wa Jiji la Arusha (CHADEMA) amesema Mbunge wa jimbo hilo Godbless Lema hataki mtu mwenye uwezo mkubwa katika chama na mara zote humpiga vita.

Naye Diwani wa Kata ya Terati  Meng'oriki amesema CHADEMA ni chama cha kihalifu, kifitini na kilichojaa chuki, ubaguzi, urasimu mkubwa huku akidai endapo ikitokea makada wa chama hicho wakimsifia Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya huwa wanakemewa vibaya.

Kwa upande mwingine, Katibu wa CCM wilaya ya Arusha Musa Matoroka amesema madiwani hao wameamua kujiunga na CCM ili kumuunga rais mkono na kuahidi kushirikiana na wananchi hao na kuwataka vigogo wa CHADEMA kuacha kupiga propaganda na siasa za uchwara kuwa kila diwani anayehama chama hicho amenunuliwa.