Jumapili , 22nd Jul , 2018

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewaagiza viongozi wa Mkoa wa Mara na Wilaya ya Musoma kuchunguza tuhuma zinazohusisha kumbi za starehe wilayani humo kuruhusu watoto walio chini ya miaka 18 kuingia na kutumia vilevi ndani ya kumbi hizo.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ametoa agizo hilo alipotembelea Mkoa wa Mara katika ziara ya kikazi ambapo alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kuwepo kwa kumbi za starehe zinazowaruhusu watoto walio chini ya umri wa miaka 18 na kutumia pombe wakiwa ndani ya kumbi hizo.

Dkt. Ndugulile amesema kwamba wamiliki wa kumbi hizo wanakiuka sheria ya mtoto, hivyo wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria mapema iwezekanavyo ili kuwalinda watoto hato chini ya umri wa miaka 18.

Aidha kwa mujibu wa wa kifungu cha 17 cha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 kinasema mtu ambaye ni mmiliki au anayeendesha au ni msimamizi wa ukumbi wa muziki, 'Bar', au klabu ya usiku hatamruhusu mtoto kuingia katika maeneno yao.

Katika kifungu imeelezwa  kuwa "mtu atakayekiuka kifungu hiki atakuwa ametenda kosa na atakapotiwa hatiani atalipa faini ya kiasi kisichopungua Shilingi millioni moja na kisichozidi Sh millioni tano au kifungo kisichozidi miezi 12 au vyote kwa pamoja".

Baada ya agizo hilo kutoka wizarani, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Bw. Adam Malima amesema ataendelea kuwachukulia hatua wale wote wanaofanya vitendo hivyo pamoja na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za Utotoni ambazo zinashamiri katika mkoa huo.