Jumanne , 12th Nov , 2019

Leo Novemba 12, miaka 81 iliyopita alizaliwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa,huko Ndanda, mkoani Mtwara, ambapo leo pia amezindua kitabu kinachoelezea maisha yake yote, tangu kuzaliwa kwake na safari yake ya uongozi

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa.

wa kulitumikia Taifa katika nyadhifa mbalimbali, alichokipa jina la 'Maisha Yangu Kusudio Langu'.

Miongoni mwa matukio makubwa ambayo ameyaeleza katika kitabu hicho, yapo yenye furaha, huzuni, uchungu na yenye kuchekesha kidogo, miongoni mwa tukio kubwa ambalo hawezi kulisahau ni lile lililotokea mwaka 1947, akiwa na umri wa miaka 9 pekee baada ya Mama yake mzazi, Bibi yake pamoja na Bibi wa Mama ake, kushambuliwa na wananchi wenye hasira kali kwa kuhusishwa na imani za kishirikina kwa madai ya kwamba wao ndiyo wamechelewesha mvua kunyesha hali iliyoleta ukame kijijini hapo.

Akisimulia kwa ufupi vipengele vinavyopatikana ndani ya kitabu hicho, mbele ya hadhara ya watu waliojitokeza katika uzinduzi, Mgoda wa Kigoda cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mkandala, amesema sehemu ya kwanza ya kitabu hicho imebeba mashujaa wawili ambao ni Bi Stephania na Mzee Matwani, ambao ni wazazi wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa.

"Wazazi hawa wawili ndiyo vinara na mashujaa wa sehemu hii ya kwanza ya simulizi hii, waliishi pamoja kwa uadilifu na heshima kubwa na mapenzi ya pamoja kwa watoto wao, ingawa wazazi hawakwenda shule lakini walipenda sana watoto wao waende shule, pamoja na kwamba Baba Matwani alikuwa na kipato kidogo lakini cha uhakika kila mwezi" amesimulia Profesa Mkandala.

Aidha Profesa Mkandala aliendelea, "kipato hicho kiliifanya familia ionekane iko tofauti hapo kijijini, hali iliyopelekea chuki na wivu, uliosababisha tukio moja baya sana, mwaka 1947 kulitokea ukame mkali, basi watu wakamleta mganga wa kienyeji akaamua kuwa, Mama mzazi,Bibi na Bibi wa Mama yake mzazi ndiyo waliroga kuzuia mvua, walipigwa na kuteswa sana hadi padre mzungu alipofanikiwa kuwanasu, Bibi wa Mama aliaga dunia muda mfupi baada ya tukio hilo"

Akisimulia safari ya masomo ya Rais Mstaafu, katika Chuo Kikuu cha Makelele, kilichopo nchini Uganda, alikumbana na mambo mbalimbali ikiwemo kugombea nafasi ya urais ya serikali ya wanafunzi, ingawa hakushinda lakini watoto wa kike walimpigia kura nyingi.

"Alishiriki siasa akiwa hapo chuoni, aligombea urais wa Serikali ya wanafunzi ingawa hakushinda, wanafunzi wa kike walimpigia kura nyingi si kwa sababu alikuwa na rafiki wa kike bali alikuwa anaweza kujieleza vizuri kuliko mpinzani wake, aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Serikali ya wanafunzi na hatimae aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa baraza la uwakilishi la wanafunzi chuoni hapo" amesimulia Profesa Mkandala.

Akizungumzia safari yake ya uongozi, hakuacha kumtaja Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwamba alikuwa ni jasiri, msikivu na alikuwa si mtu wa kumkatiza mtu hata kama anaongea pumba na kwamba Mwalimu alikuwa ni Mwalimu wake wa kila kitu.