Jumatatu , 11th Nov , 2019

Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James, ameziagiza taasisi za manunuzi za Serikali kuhakikisha hadi kufikia Desemba 31, 2019, ziwe zimejiunga na Mfumo wa manunuzi ya Umma kwa njia ya kielektroniki (TANePS) na kwamba baada ya tarehe hiyo hakuna taasisi itakayoruhusiwa kufanya

Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James.

manunuzi bila kutumia mfumo huo.

Hayo ameyabainisha leo Novemba 11, 2019, wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa Fedha, kuhusu matumizi ya mfumo huo kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa umma(PPRA), amesema kuwa toka mfumo huo uanze tayari taasisi za umma 418 kati ya 540  zinazojihusisha na manunuzi zimekwisha unganishwa.

"Mfumo huu utasaidia kuondoa mambo mengi ya gizani yaliyokuwa yakiendelea na mambo mengi yaliyokuwa yakichelewesha kwa ile kauli ya michakato michakato, ile habari ya kuzunguka nyuma ya nyumba unaongea na watu halafu baadae unakuja kuwatengenezea mazingira dawa yake ndiyo hii, waliokuwa wakiishi kwa rushwa kupitia manunuzi hawa ndio tunaenda kukabiliana, mfumo huu utatibu ugonjwa mwingine uliokuwa umejikita kwenye sekta ya manunuzi" amesema Katibu Mkuu.

Aidha Katibu Mkuu Dotto James, ameongeza kuwa endapo taasisi zote za umma zitaunganishwa katika mfumo huo, Serikali itakuwa imeokoa kiasi cha shilingi bilioni 34, zinazotumika katika matumizi yasiyokuwa na tija, ikiwemo uchapaji wa nakala, usafirishaji pamoja na vikao mbalimbali.