Ijumaa , 24th Jan , 2020

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa tahadhari ya mlipuko wa ugonjwa wa homa ya mafua makali, unaosababishwa na kirusi kipya jamii ya Corona, uliozikumba Nchi za China, Thailand, Japan, Korea Kusini na Marekani kuanzia mwanzoni mwa mwezi Disemba 2019.

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoo, Ummy Mwalimu

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara, imeeleza kuwa tayari imekwishaanza kuchukua hatua za kukabiliana na tishio la ugonjwa huo ikiwemo, kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huo, kupima sampuli, kuwataka Waganga wa Wakuu wote kuchukua tahadhari na kuimarisha ufuatiliaji, kuandaa maeneo maalumu ya matibabu endapo mgonjwa atajitokeza pamoja na kuandaa vifaa kinga.

"Ugonjwa huu huambukizwa kwa njia ya hewa kwa kuingiwa na majimaji yenye virusi, kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya kukohoa au kupiga chafya au kwa kugusa majimaji au makamasi kutoka kwa mgonjwa aliyethibitishwa" imeeleza taarifa hiyo.

Takwimu za mlipuko wa ugonjwa huo zinaonesha kuwa hadi kufikia januari 22, 2020, watu wapatao 560 wameathirika huku vifo vikiwa ni 17, ambapo Nchi ya China imethibitisha wagonjwa 550 na vifo 17.