Jumatano , 22nd Jan , 2020

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesema kuwa hadi sasa hivi haijapokea waraka wowote wa Kidplomasia kutoka nchini Marekani, unaoeleza kuwa Nchi ya Tanzania ni miongoni mwa Nchi ambazo zitawekewa vikwazo kwa raia wake kwenda nchini Marekani.

Bendera ya Tanzania na Marekani.

Akizungumza leo Januari 22,2020 na EATV&EA Radio Digital, Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Emmanuel Buhohela, amesema kuwa hayo yanayoendelea ni maneno ya mitandaoni tu kutokana na kwamba wao hawajapata waraka wowote.

"Sisi kama Wizara mawasiliano yote huwa yanafanyika kwa Waraka maalumu wa Kidplomasia, ndio maana kuna Ubalozi kwahiyo kama kungekuwa na jambo lolote wangetueleza kwa  kutumia njia hiyo, na hadi sasa hatujapata ujumbe wowote na hatuwezi kuzungumzia vitu ambavyo vinasemwa kwenye mitandao" amesema Buhohela.

Taarifa za kwamba Serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani kuwa na mpango wa kuziongeza Nchi nyingine 7, ikiwemo Tanzania kwenye orodha ya Nchi ambazo, Raia wake wamewekewa vikwazo vya kuingia nchini humo, zimeanza kusambaa leo katika mitandao mbalimbali ya kijamii.