Jumatatu , 15th Oct , 2018

Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe amekuwa akimshinikiza Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema kutoa maoni mbadala juu ya taarifa iliyotolewa na Waziri husika, Kangi Lugola juu ya matukio mbalimbali yanayotajwa kuwa ni ya utekaji.

Zitto Kabwe

Zitto ameonekana kushikilia msimamo huo hata katika andiko lake la pili baada ya lile alilolitoa hivi karibuni kufuatia tamko la Waziri Lugola ambalo alinukuliwa akisema katika kipindi cha miaka 3 watu 75 walisadikika kutekwa.

Kupitia ukurasa wake wa twitter, Zitto Kabwe  ameandika "ndugu@godbless_lema kwenye utamaduni wa Jumuiya ya Madola, Waziri mwenye dhamana akitoa kauli, lazima Waziri Kivuli wa sekta hiyo atoe kauli pia, ama kuunga mkono au kupingana na ya Waziri mwenye dhamana".

Zito ameongeza, "tunasubiri kauli yako. Nchi inasubiri. Kukaa kimya nikukubaliana na Kangi" 

Hivi karibuni kupitia ukurasa wake wa Twitter, Mbunge na Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi aliandika ujumbe ukionesha analifatiliatukio la kupotea kwa Mfanyabiashara Mohamed Dewji.

"Nafikiri kwa sasa ninaweza kuongea na waandishi wa habari kuhusu kutekwa kwa mfanya biashara Mo Dewji", ameandika Lema.