"Zitto mshirikina, Mbowe anauguliwa - Makonda

Jumanne , 24th Mar , 2020

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, amewataka wananchi kusikiliza kauli za Serikali juu ya namna gani watajikinga na kupata maambukizi ya Virusi vya Corona na waachane na wanasiasa kama kina Mbowe kwa sababu wao wanangoja ndugu zao waugue na wao ndio wasitishe mikutano yao.

Mbunge Zitto Kabwe, Freeman Mbowe na RC Dar es Salaam Paul Makonda.

Makonda ameyabainisha hayo leo Machi 24, 2020, wakati wa ziara yake maalum katika stendi ya Mabasi yaendayo mkoani ya Ubungo.

"Tusikubali kupokea ushauri na ushawishi wa wanasiasa uchwara kama kina Mbowe kwa sababu asingeugua mtu wa familia yake aliyetoka nje akaja na huo ugonjwa mngeingizwa kwenye mikutano na kuleta mvutano na Dunia ingeona Tanzania haina demokrasia, mkiacha kuwasikiliza watalamu wa afya na kuwasikiliza waganga wa kienyeji na washirikina kama kina Zitto Kabwe kazi kwako" amesema Makonda.

Jana Machi 23, 2020, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, alitangaza kusitisha kufanya mikutano yake ya hadhara nchi nzima, ambayo alitangaza kuianza Aprili 4.