Jumatatu , 15th Feb , 2021

Watu 60 wakazi wa wilaya ya Rombo wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Kilimanajaro kwa tuhuma za utengenezaji wa pombe haramu ya gongo na usafirishaji wa madawa ya kulevya aina ya bangi na mirungi.

Katikati ni Mkuu wa operesheni maalumu za jeshi la polisi Tanzania kamishna msaidizi mwandamizi Mihayo Msikhela na Kushoto ni Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa kilimanjaro Ronald Makona

Mkuu wa operesheni maalumu za jeshi la polisi Tanzania kamishna msaidizi mwandamizi Mihayo Msikhela amesema watu hao wamekamatwa na lita 500 za pombe haramu ya gongo na zaidi misokoto 2300 ya bangi.

"Tumefanikiwa kukamata watuhumiwa takribani 60 vielezo vilivyopatikana ni gongo ambayo ni lita 549.2 , mitambo ya kutengeneza gongo ambayo ni 18, mapipa matupu 112, pikipiki 4, madumu tupu 38  ya lita 20 yenye rangi ya njano, ndoo mbili tupu za lita 20 , mirungi kilo 68.8, misokoto ya bangi 2340, mazao ya misitu ambayo ni mbao 497" amesema kamishna msaidizi mwandamizi Mihayo

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa kilimanjaro Ronald Makona akazungumzia zoezi hilo ambalo amesema ni endelevu kwa wilaya zote za mkoa wa kilimanjaro na tiyari wana majina ya watu amabo wanaendelea kuwaorodhesha kwenye orodha yao na wataendelea kuwasaka mpaka pale watakapopatikana.