Jumapili , 21st Feb , 2021

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewashukuru Watanzania wote kwa kutekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli la maombi ya siku tatu kuliombea taifa dhidi ya janga la corona, na imewasisitizia Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Bw. Gerard Julius Chami

Agizo hilo lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kuanzia tarehe 19/02/2021, siku ya Ijumaa alipokuwa kwenye ibada ya kuuga mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi ambapo aliwataka Watanzania kutokuwa na hofu na kumtegemea Mungu.

Taarifa ya Wizara ya Afya iliyotolewa leo kupitia ukurasa wao imepongeza madhehebu yote, viongozi wa dini na wadau mbalimbali kwa kutekeleza maombi hayo kwa moyo wa dhati na kutoa rai kwa Watanzania kuendelea kumuomba Mungu na kuchukua tahadhari za afya na kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya.

Aidha, Wizara imewasisitizia wananchi kuzingatia tahadhari zote ikiwemo, unawaji wa mikono mara kwa mara kwa kutumia maji tiririka, kutumia vipukusi (sanitizer), kufanya mazoezi, lishe bora, uvaaji wa barakoa sambamba na kuwalinda wazee na wale wenye magonjwa ya muda mrefu.