Jumatatu , 24th Sep , 2018

Mkurugenzi Mkuu wa Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’, Asha Baraka amesherehekea 'birthday' yake 'weekend' hii bila kukata keki, huku akidai sababu kubwa ni msiba uliotokana na ajali ya kivuko cha MV. Nyerere mnamo Septemba 20, 2018 mkoani Mwanza.

Asha Baraka

Asha Baraka ameeleza hayo alipokuwa anazungumza na eNewz na kusema amepokea kwa huzuni kubwa taarifa ya ajali hiyo na ndio iliyomsababisha kutokata keki kwasababu ya huzuni aliyokuwa nayo.

"Nimepata zawadi chache zikiwemo keki mbili, ambazo moja nimepewa na wadau wa muziki wa Twanga na nyingine kutoka kwa binti wa filamu lakini sitaweza kuzikata kutokana na kuzama kwa MV. Nyerere, na baadhi ya fedha ambazo nimechangiwa nusu nitazitoa kwenye mchango wa maafa ili mradi tu kuwasaidia wezetu huko Mwanza", amesema Asha Baraka.

Kwa upande wake, Thea ambaye ni muingizaji wa filamu nchini amesema kwamba Asha Baraka amekuwa ni kama maama yao kwani anawafundisha mambo mengi juu ya sanaa hivyo nilazima awe naye katika siku yake ya kuzaliwa, huku akidai ameshasahau masuala ya ndoa kwa sasa na anaishi maisha yake bila ya kukumbuka chochote kile kinachohusu ndoa.

Ajali ya kivuko cha MV. Nyerere imetokea Septemba 20, 2018 katika Ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watanzania takribani 224 ambao wamezikwa katika makaburi ya pamoja yaliyopo viwanja vya shule ya sekondari ya Bwisya mita 250 kutoka gati la Bwisya.

Hadi sasa serikali imeshaanza kuchukua hatua stahiki kwa mamlaka husika juu ya tukio hilo, licha ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuunda rasmi tume ya uchunguzi ambayo inaongozwa na Jenerali Mstaafu George Waitara kama Mwenyekiti wa tume hiyo, na wamepewa muda wa mwezi mmoja ili tume hiyo itoe majibu na  mapendekezo juu ya hatua ambazo serikali inapaswa kuzichukua.