Alhamisi , 25th Apr , 2019

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Susan Mlawi ameagizwa ampangie kazi nyingine Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza, Bi. Joyce Fisoo na ateue mtu mwingine kushika nafasi hiyo. 

Kutoka kulia ni Joyce Fisoo akizungumza na Wema Sepetu ambaye alikuwa na Katibu wake Neema Ndepanya katikati

Agizo hilo lilitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wakati akihitimisha kikao chake na wasanii zaidi ya 100 kutoka Shirikisho la Filamu Tanzania kilichofanyika ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma. 

Kikao hicho ambacho kilidumu kwa zaidi ya saa saba, kilihudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bodi ya Filamu Tanzania pamoja na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wakiongozwa na Naibu Waziri wa Habari, Juliana Shonza.

 “Katibu Mkuu mtafutie eneo jingine la kufanya kazi. Hana tuhuma zaidi ya mahusiano mabaya na wadau wake, ana historia nzuri, lakini tatizo ni mahusiano. Mpeleke idara nyingine na hapa mlete mtu mwingine", ameagiza Waziri Mkuu.

Amesisitiza kuwa, "Mama Fisoo wewe uko 'clean', sina tatizo na utendaji wako lakini ukikaa hapa hutaweza kwenda mbele na wala hawa wote hawatakuja kufanya kazi na wewe. Tunataka hii tasnia iende mbele, tunataka maendeleo kwenye tasnia ya filamu".

Shirikisho la Filamu Tanzania linajumuisha vyama 11, ambapo 10 vimesajiliwa na kimoja hakijakamilisha usajili. Vyama hivyo ni vya waigizaji, waongozaji, watayarishaji, wahariri, wachekeshaji na wapigapicha. Wengine ni waandishi wa miswada (script writers), watafutaji mandhari, wasambazaji wa filamu, walimu na chama cha wanawake wa tasnia ya filamu ambacho bado kiko kwenye mchakato wa usajili.

Joyce Fisoo alimfungia Wema Sepetu kwa muda wa miezi kadhaa baada ya kuvuja kwa picha zake za faragha mtandaoni, kitendo kilichoonesha kutowafurahisha wasanii wa filamu ambao mwishoni mwa wiki iliyopita walikuwa na kikao cha dharura wakishinikiza aondolewe.