Jumatano , 11th Jul , 2018

Raisi wa Bodi ya filamu Tanzania (TFB), Simon Mwakifamba amesema kuwa zao la waigizaji chipukizi kwenye tasnia ya filamu ni kubwa kuliko kwenye muziki kwa madai ya kuwa filamu zilizofanywa na waigizaji hao ni nyingi lakini jambo linalowakwamisha chipukizi hao kuonekana ni ugumu wa mauzo.

Raisi wa Bodi ya filamu Tanzania (TFB), Simon Mwakifamba.

Mwakifamba amezungumza hayo wakati akiongea na www.eatv.tv  na kubainisha kuwa katika wanamuziki chipukizi ni mmoja mmoja sana anaekwenda studio kurekodi na kusimama kama ‘solo artist’ tofauti na kwenye filamu ambayo hutoa nafasi kubwa ya kuwahusisha waigizaji chipukizi wengi kwa wakati mmoja. Licha ya kukabiliwa na changamoto ya filamu walizoshiriki kutopenya kwenye soko la filamu kwa sababu ya poromoko la mauzo ya filamu kwenye tasnia hiyo.

"Tasnia ya filamu inahusisha wahusika wengi, lakini wasanii wa muziki husimama peke yake kwenda studio na kuimba kama ‘solo artist'. Changamoto iliyopo ni kwamba filamu nyingi zinatengenezwa lakini soko halijakaa vizuri, jambo linalosababisha filamu zinazoingia sokoni kuwa chache hivyo ile fursa na nafasi ya waigizaji wenye vipaji vyao kuonekana inakua ndogo", Mwakifamba.

Aidha Katibu Mkuu wa Chama cha Muziki wa kizazi kipya (TUMA) aliyefahamika kwa jina moja la Brighton amekiri kutokuwepo kwa takwimu za kubaini wanamuziki wanaochipukia na kuweka wazi kuwa kwa sasa ndiyo wapo mbioni kuanza mpango huo wataofanya kwa kushirikiana na kampuni ambayo tayari wameshafanya makubaliano nao ya kuzunguka nchi nzima kupata takwimu hizo.

"Tayari tumeshafanya maongezi na kuingia mkataba na kampuni, ambayo ikiwa tayari ndipo tutaanza rasmi mchakato wa kubaini idadi kamili ya wanamuziki chipukizi na wale wanatoa kazi zao kwa ujumla nchini kote", amesisitiza Brighton.