Alhamisi , 19th Apr , 2018

Msanii chipukizi wa muziki wa hip hop bongo ambaye anazidi kupanda chati kwa ngoma zake kali, Clicker, ameitaka serikali kuwapa uwezo wasanii kufanya kazi zao kwa urahisi zaidi, ili kuweza kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza na www.eatv.tv Clicker amesema wasanii wanapata changamoto nyingi sana kutoka serikalini licha ya jitihada wanazozifanya kuweza kujikwamua kiuchumi kupitia sanaa, hivyo ni wakati sasa wa kuwapa msaada zaidi ili waweze kufanikisha kazi zao na kuchangia pato la nchi.

Clicker amesema mara nyingi wanapata ugumu wanapotakiwa kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya kazi zao za sanaa kwa kuchelewa kupata hati za kusafiria pamoja na vibali vingine, hivyo hukwamisha baadhi ya mambo.

Serikali ituunge mkono kwenye hizi kazi zetu, tunapata changamoto sana, kuna vitu kama msanii nashindwa kufanya hapa nyumbani kutokana na sheria zilizopo, hivyo itusaidie kuweza kufanikisha hayo mambo kama kupata passport kwa haraka unapohitaji kusafiri, kuturaisishia mazingira yetu ya kazi na pia itupe uhuru wa kutoa maoni”, amesema Clicker.

Msanii huyo hivi karibuni ameachia kazi mpya akiwa na msanii mwenzake Bright, inayojulikana kama 'hawatudai'.