Jumatatu , 17th Jul , 2017

Msanii Darassa amesema kwamba katika maisha yake anatembea kupitia darasa la Prof. Jay hata kama hataweza kuwa mbunge atajitahidi kuishi kwenye misingi iliyo imara.

Akizungumza Jumapili hii kwenye tafrija iliyoandaliwa na Prof Jay kwenye jimbo la Mikumi, Darassa amesema kwamba tangu ameanza kumjua nguli huyo wa hip hop bongo na kumfuatilia amekuwa nguzo kubwa ya kumuongoza na jinsi ya kutokubali kushindwa.

"Prof Jay ni mtu ambaye amekuwa na ushawishi mkubwa sana kwangu. Alianza kupigania huu muziki kuanzia bahari ya muziki wa bong fleva haiko sawa na sasa hivi imetulia ametuachia wadogo zake, lakini pia ametuonesha siyo muziki tu hata unaweza kuwa kiongozi na watu wakakupatia heshima akawa mbunge na sasa hivi tunasherehekea harusi yake amekuwa baba wa familia. Kwa upande wangu nitazidi kujifunza kupitia Jay hata kama sitakuwa Mbunge lakini nitaishi katika misingi kama ya kwake", alisema.

Akizungumzia jinsi Prof alivyoweza kumtambua kama msanii darassa amesema kwamba

"Madini siku zote yanajuana. Kwa mara ya kwanza nilimsikia Prof akinisifia kwenye redio kipindi mimi nikiwa bado mtaani nahangaika kupata nafasi nikiwa na wimbo mmoja wa 'Sikati Tamaa' na alinitabiria makubwa na hata siku naonana nae alinitia nguvu sana ndio maana nasema atazidi kuwa Mwalimu wangu" Darassa