Familia ya Ruge yaomba radhi, yatoa msamaha

Jumamosi , 2nd Mar , 2019

Familia ya Ruge Mutahaba imewataka watu waliowahi kukosewa na ndugu yao Ruge Mutahaba kumsamehe, kwani naye alikuwa binadamu asiyekamilika.

Akizungumza kwa niaba ya familia mtoto mkubwa wa Marehemu, Mwachi Mutahaba, amesema kwamba wanatambua kuwa baba yao alikuwa ni mfanya biashara, na kwa namna moja au nyingine anaweza akawa amewakosea watu, hivyo wanaomba wamsamehe ndugu yao aende kwa usalama, na pia wao kama familia wamewasamehe wale waliomkosea.

"”Kama binadamu tunatambua kuna wale aliowakwaza kwa namna moja au nyingine, kwa niaba ya familia tunaomba mumsamehe, na sisi kama familia tunawasamehe wale ambao kwa namna moja au nyingine walimkosea". Amesema Mwachi Mutahaba.

Hii leo mwili wa Ruge Mutahaba ueagwa katika uwanja wa Karimjee, huku ukihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kitaifa, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na wengineo.