Familia yazungumza juu ya kifo cha Ruge

Jumatano , 27th Feb , 2019

Familia ya Marehemu Ruge Mutahaba ambaye amefariki dunia hapo Jana nchini Afrika Kusini, imeweka wazi kilichotokea mpaka Ruge akakutwa na mauti, akiwa hospitali akiendelea na matibabu ya figo ambayo ilikuwa ikimsumbua,

Mwombeki Baregu ambaye ni ndugu wa Ruge Mutahaba amesema kwamba jana asubuhi Ruge aliamka huku presha yake ikiwa haiko sawa, lakini licha ya madaktari kufanya jitihada zao ili kumuweka sawa, ilishindikana na kusababisha kupoteza maisha.

Asubuhi leo (jana) ndugu yetu Ruge Mutahaba, aliamka katika hali ambayo presha yake ilikuwa haijatulia, madaktari na wasaidizi wengine wa hospitali walijaribu kumsaidia, lakini mnamo saa 10:30 Jioni kwa saa za South Afrika au saa 11:30 kwa muda wa hapa nyumbani, ndugu yetu Ruge Mutahaba, alifariki akiwa na mdogo wake na watu wa dini ambao walikuwepo naye”,amesema Mwombeki.

Mwombeki ameendelea kwa kusema kwamba utaratibu wa kurudisha mwili wa marehemu unaanza kufanyika, huku akiwashukuru watu waliojitokeza kuifariji familia yao.

“Na kwa sasa familia inashukuru watu amabo wamefika hapa kutufariji kwa muda mfupi, na utaratibu wa kuangalia namna ya kumrudisha ndugu yetu nyumbani kwa ajili ya mazishi ndio zinaanza, kesho (leo) tutakuwa tunafahamu zaidi kuhusu huo utaratibu na kuweza kutoa taarifa rasmi ya utaratibu na mazishi”, amesema Mwombeki.

Ruge Mutahaba alikuwa mmoja wa waasisi wa Clouds Media Group na mmoja ya watu aliochangia kukuza sanaa ya bongo kwa kuibua wasanii mbali mbali, na atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa kwenye maisha ya vijana wengi.

Ruge alianza kusumbuliwa na tatizo la figo mwishoni mwaka 2018 ambapo alilazwa katika hospitali ya Kairuki, na baadaye kuhamishiwa nchini Afrika Kusini ili kupata matibabu zaidi, mpaka kifo kilipomkuta Februari 26, 2019.