Jumatano , 21st Mar , 2018

Malkia wa muziki wa Taarab Afrika Mashariki na kati kama anavyojiita mwenyewe, Khadija Omar Kopa, ameweka wazi juu ya tukio lake alilowahi kufanya wakati yupo kijana la kutoa mimba, na kwamba anajutia kwa maisha yake yote.

kizungumza kwenye kipindi cha #KIKAANGONI kinachorushwa kupitia ukurasa wa facebook wa East Africa Television, Khadija amesema mimba hiyo aliipata akiwa kijana na akiwa kwenye chati, hivyo akaona itamuharibia mipango na kuamua kutoa, lakini ni jambo analomuomba Mungu amsamehe kwani si jambo zuri kulifanya.

“Najuta kwweli kweli wakati ule ndio jina limesimama kweli kweli na mimba wapi na wapi, ukute mwanangu angekuwa rais sasa, namuomba Mungu anisamehe, najuta sana na vijana msifanye hilo. Mungu naomba anisamehe sitaki kulisikia tena jambo hilo”, amesema Khadija Kopa.

Khadija Kopa ameendelea kwa kuwataka mabinti kutofanya jambo hilo na kujiepusha nalo, kwani ni ujinga na siyo kitu kizuri.

“Kutoa mimba ni ujinga sana, maana saizi ningekuwa na watoto wangu kama saba, hivyo mabinti zangu nawashauri msije kutoa mimba kwani ni kitu kibaya sana”, amesema Khadija Kopa.