Lulu asherehekea 'birthday' MOI

Jumatatu , 16th Apr , 2018

Msanii wa filamu Bongo ambaye kwa sasa anatumikia kifungo chake cha miaka miwili gerezani Segera, Elizabeth Michael (Lulu) , ameadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kutoa misaada kwa watoto wenye matatizo ya vichwa vikubwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili Taasisi ya Mifupa (MOI).

Akizungumza kwa niaba yake, msanii mwenzake ambaye pia ni mtu wa karibu wa familia ya Lulu, Mahsein Awadh maarufu kama Dkt. Cheni, amesema kwamba amepewa ujumbe kutoka kwa Lulu akisema kwamba anafahamu mama yake ana machungu sana kwa kipindi hiki ambacho yupo kwenye matatizo, hivyo wazazi wa watoto hao ambao anawaptia misaada leo watakapofarijika, ana imani na mama yake atafarijika pia.

“Siku ya leo ni siku ya kuzaliwa kwa Lulu akaona ijumuishe kuleta vitu hapa hospitali, anapenda kutoa zawadi ndogo, anaamini hawa wamama wana machungu sana, hata yeye mama yake amepata machungu mengi sana kwa kipindi hiki ambacho yupo kwenye matatizo, anaamini wamama hawa watakapofarijika na watoto wao, faraja hiyo atakuwa anaipata na mama yake mzazi”, amesema Dkt. Cheni kwa niaba ya Lulu.

Dkt. Cheni ameendelea kwa kusema kwamba Lulu amewataka wamama hao kuomba Mungu ili watoto wao waweze kupona, na kwamba anawakumbuka sana na kuwapenda watu wote, huku akiwaomba waendelee kumuombea.

“Amesema anaamini kwa kumuomba Mungu haya maradhi yanayowakabili yatapona kwa muda mfupi, anapenda kuwashukuru kwa siku ya leo, ambayo ameona atoe zawadi hii, anawapenda na anawakumbuka marafiki , ndugu na jamaa wote anaomba muendelee kumuombea”, amesikika Dkt. Cheni.

Msanii Elizabeth Michael alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela hapo Novemba 13, 2017, kwa kosa la kumuua bila kukusdia msanii mwenzake Steven Kanumba, ambaye alikuwa naye kwenye mahusiano kwa siri.