Ijumaa , 11th Oct , 2019

Mwenyekiti wa Umoja wa Mabaunsa Tanzania, Faraj Robert amesema kauli ya Ney wa Mitego juu ya suala la wao kuwalinda watu maarufu hawajaielewa kwakuwa wao wana vigezo vyao wanavyozingatia ili kufanya kazi.

Mabaunsa katika siku ya kmbukumbu ya kuzaliwa ya Irene Louis (officiallyyn)

Amesema hayo alipokuwa akipiga stori na Big Chawa wa Planet Bongo ya East Africa Radio, ambapo amesema Ney wa Mitego hawezi kueleweka kwa sababu anaonekana ana nia ya kuidhihaki tasnia ambayo inasaidia ulinzi wa watu.

"Kauli za Ney haziwezi kueleweka, huwezi ukaikashifu tasnia ambayo inakupa ulinzi wako, familia na mali. Huwezi tu ukasema mabaunsa tuko 'cheap' bei rahisi", amesema Mwenyekiti huyo.

"Sisi vigezo vyetu ni mtu akiwa na pesa tu tunamlinda kwa sababu ni binadamu na anahitaji usalama. Suala lingine tunalizingatia ni mazingira ya kufanya kazi", ameongeza.

Hivi karibuni msanii wa Hip Hop Bongo, Ney wa Mitego aliandika katika mtandao wa Instagram akisema kuwa kazi ya ulinzi binafsi inadhalilishwa kutokana na mabaunsa kukubali kuwalinda watu ambao hawastahili, suala ambalo limeibua hisia kali kutoka kwa mabaunsa hao.