Jumamosi , 1st Feb , 2020

Mapema asubuhi ya leo Februari 1, 2020, zimetoka taarifa za kupata ajali ya gari kwa msanii chipukizi wa Singeli Meja Kunta, maeneo ya Segera mkoani Tanga wakati anatokea Dar es salaam kwenda kufanya show huko.

Kushoto ni Meja Kunta, kati Man Fongo, kulia ni Madee

EATV & EA Radio Digital, imewapata wasanii Madee na Man Fongo ambao walikuwepo eneo la tukio na wamenyoosha maelezo kuanzia ajali ilivyotokea, chanzo na kinachoendelea kwa sasa.

"Nilikuwa napita na safari zangu nikaukuta huo msala barabarani, nilichokifanya ni kusaidia kumuhamisha kwenye gari na kuwahishwa Tanga hospitali, wametoka Dar kuja huku walivyofika maeneo ya Segera nafikiri dereva wao alikuwa na usingizi na gari ikahama na kutumbukia chini kwenye bonde, Meja Kunta ndiyo alikuwa siriazi sana maana ameumia mbavu" amesema Madee.

Kwa upande wa msanii mwenzake wa Singeli Man Fongo, akizungumzia tukio hilo ameeleza kuwa  "Kwa kweli amepata ajali tulikuwa tunaenda kufanya show Tanga, mimi niliwahi kufika nikawaacha nyuma ila nikapigiwa simu kwamba wamepata ajali ndiyo tukarudi eneo la tukio, wanaendelea vizuri hakuna aliyepata majeraha makubwa ila wameumia ndani kwa ndani, ajali imetokea mida ya saa 10:00 kuelekea Saa 11:00 Alfajiri".