Jumatano , 11th Jan , 2017

Mume wa mwanamuziki wa Injili Flora anayefahamika kwa jina la Emmanuel Mbasha amefunguka na kuweka wazi kuwa amekuwa akihangaika sana kuhakikisha mkewe huyo anarudi nyumbani na kuendelea kuishi kama zamani lakini jitahada zake zimegonga mwamba.

Flora na Emmanuel Mbasha

Emmanuel Mbasha akiongea kwenye kipindi cha eNEWZ alisema kuwa toka mkewe huyo ameanzisha songombingo hilo yeye alikuwa anahitaji mambo hayo yaishe ili mwisho wa siku waishi vizuri tena kama mume na mke kwani yeye hakujiandaa wala kujipanga kuachana na mkewe huyo.

"Kiukweli toka mwaka 2014 nimekuwa nikimbembeleza sana Flora arudi nyumbani, hata niliposhinda kesi nilikuwa namtumia jumbe mfupi kumtaka arudi ili tuishi kama zamani lakini wapi, kila vikao vya usuluhishi vilipoitishwa mwenzangu alikataa, lakini kiukweli kabisa nilikuwa natamani tuendelee kuishi wote kwani tayari tuna mtoto mmoja na mimi sikuwa tayari wala sikujipanga kuachana na Flora na wala sikufikiria kuwa ipo siku nitakuja kuachana naye" alisema Emmanuel Mbasha 

Mbali na hilo Emmanuel Mbasha amemtaka mkewe huyo kumkumbuka Mungu na kuishi katika vitu ambavyo anaviimba kwenye nyimbo zake za Injili kwani yeye ni kioo cha jamii na mtumishi wa Mungu pia.