"Mimi msanii wa RockStar siyo Alikiba" - Baraka

Jumanne , 11th Jul , 2017

Msanii Baraka The Prince ambaye yupo chini ya usimamizi wa kampuni ya RockStar4000 amefunguka na kusema kuwa yeye ni msanii aliye chini ya usimamizi wa RockStar4000 na si msanii aliye chini ya Alikiba.

Msanii Baraka The Prince

Baraka The Prince amesema hayo kupitia kipindi cha 5 Selekt na kusema yeye anatambua kuwa Alikiba sasa amekuwa Director wa kampuni hiyo na anaamini anaweza kufanya vizuri lakini yeye hana taarifa zozote juu ya mchongo huo ambao ameupata Alikiba kwenye uongozii wake huo. 

"Mimi sitaki sana kuzungumzia sana juu ya Alikiba kuwa Director wa RockStar4000 kwani kipindi ambacho yeye anaingia mikataba mimi nilikuwa Nairobi na wao walikuwa Afrika Kusini na sijapata nafasi kusikia chochote hivyo kwa sasa bado sijui vizuri hilo jambo, siwezi kulizungumzia japo nafahamu maana naweza kuzungumzia nikazungumza nikasema jambo lisilo la kweli. Ila nimefurahi sababu Alikiba ni kaka yangu na naishi naye vizuri na najua kuwa kazi itakwenda vizuri". Amesema Baraka The Prince 

Mbali na hilo Baraka The Prince alitoa ufafanuzi kuwa yeye ni msanii anayesimamiwa kazi zake na kampuni ya RockStar4000 na si kusimamiwa na Alikiba kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakidhani au wakihisi hivyo. 

"Mimi ni msanii wa RockStar4000 na si msanii wa Alikiba hilo watu naomba waelewe" alisema Baraka The Prince 

Kwa kumalizia Baraka The Prince alisema watu wengi wanamchukia kutokana na misimamo yake katika kazi yake ya muziki na kudai wasanii wengi wa bongo wamekuwa wakifanya kazi zao kienyeji sana ndiyo maana anapishana nao, kwani yeye anataka kazi ambayo anashiriki iweze kuwekewa mipango na iende katika viwango.