Mrisho Mpoto adai mwanaye amekataa kumfuata

Jumanne , 5th Nov , 2019

Msanii wa mashairi Bongo, Mrisho Mpoto, ameeleza kuwa alipata mshtuko mkubwa baada ya mwanaye wa kiume aitwaye Manju, kukataa kufuata mienendo na kazi anazozifanya yeye.

Kupitia EATV & EA Radio Digital, Mrisho Mpoto, amesema huyo ndiyo mtoto pekee anayetegemea kwamba atakuja kufuata kile anachokifanya ila alipata mshtuko baada ya mwanaye kumwambia hatafuata njia zake.

"Mwanangu anamaliza kidato cha nne ila ndiyo mtoto pekee ambaye nilikuwa namtegemea labda angekuja kufuata kile ambacho ninakifanya kwa sababu katika makuzi yake tulikuwa tunazungumza, alikuwa ana maswali na ananifuatilia, nikawa najua kwamba ipo siku njia nilizopita na yeye atapita na alionesha kwamba anataka kunifuata" amesema Mrisho Mpoto.

Mpoto ameongeza kuwa, "Nakumbuka siku kumi kabla ya mahafali yake aliniambia nimtembelee shuleni ila alisema hana shauku na hayupo tayari kwa kile ninachokifanya, pia akasema hatatembea peku hatafanya kazi ambayo mimi ninaifanya, akabadilisha muelekeo na anataka kuwa I.T au Mwanajeshi, kwahiyo ile kwangu ilikuwa kama mshtuko"