Jumatano , 15th Aug , 2018

Mwalimu na mwanamuziki wa bongo Fleva, Barnaba Elias 'Barnaba Classic' amedai sio kweli wimbo wake mpya wa 'tuachane mdogo mdogo', ulikuwa unamlenga aliyekuwa mpenzi wake na mzazi mwenzake Zuu Namela bali anachokifahamu yeye kuwa amewaimbia watanzania waliompa dhamana ya kuimba.

Msanii Barnaba akiwa katika picha ya pamoja na aliyekuwa mpenzi wake Zuu Namela.

Barnaba amebainisha hayo leo Agosti 15, 2018 wakati alipokuwa anazungumza na www.eatv.tv ikiwa imepita siku chache tokea alipoachia wimbo wake huo, ambao tungo zake zimeonekana kwa namna moja ama nyingine zikimlenga mama Steve na kuibua mjadala mzito kwa mashabiki zake, kuwa akili yake bado ina muwaza mpenzi wake huyo licha ya kuwa wameachana muda.

"Siwezi kuzungumzia masuala ya mzazi mwenzangu. Mmeshawahi kuona wapi mtu anamuimbia wimbo mtu mmoja kila siku, mimi nawaimbia watanzania. Watu walianza kumjua Barnaba kabla ya kuingia kwenye mahusiano. Sijaanza kuimba mapenzi leo, nafanya kazi kwaajili ya watanzania ambao wamenipa dhamana ya mimi kuwepo hapa nilipo", amesema Barnaba.

Mbali na hilo, pia Barnaba amesema yupo mbioni kuachia albamu yake tatu aliyoipa jina la 'gold' huku akiwarusha dongo wasanii wenzake, waliokuwa wanalalamika kwamba albamu hailipi na kudai wao wenyewe ndio walikosea kwa kutoa albamu nyepesi nyepesi.

"Albamu yangu ya gold itaingia sokoni rasmi tarehe 31 mwezi huu na itakuwa na jumla ya nyimbo 25 kati ya hizo, tano zimeshasikika hewani. Nimeamua kuja na albamu kwasasabu ninaamini watanzania wanapenda na kuhitaji muziki mzuri. Hatuwezi kuliacha soko la albamu kwa kuhofia kuibiwa, wizi upo duniani kote", amesisitiza Barnaba.

Albamu hiyo kwa mara ya kwanza ilipangwa kutoka mwezi Februari 2018 lakini ikahairishwa hadi Juli 2018, kutokana na kile kilichoelezwa na Barnaba kuwa wadhamini wake wakuu watatu, walipendelea hivyo ambapo pia haikufanyika na badala yake kutoka rasmi Agosti 31 mwaka huu.

Gold itakuwa albamu ya tatu kwa Barnaba ambapo ya kwanza alitoa kwenye miaka ya 2009 kuelekea 2019 iliyojulikana kwa jina la njia panda na albamu yake ya pili aliiachia mnamo mwaka 2011 kuelekea 2012 iliyoitwa kisa changu.