Jumamosi , 20th Apr , 2019

Mbunge wa Geita vijijini Joseph Musukuma, ameitaka wizara ya inayoshughulika na masuala ya sanaa kuangalia namna ya kuokoa sanaa ya filamu bongo (bongo movie), kwani imekuwa ikianguka siku hadi siku, huku wasanii wake wakiishi maisha magumu.

Musukuma ametoa rai hiyo Bungeni, ambapo amesema kwamba imefikia hatua wasanii wa bongo movie wanategemea rambirambi ili kuishi, kufungua madanguro na kuwa makuwadi, na kumtaka Waziri wa Habari, Sanaa na michezo Harrison Mwakyembe kutafuta suluhu ya kuwasaidia.

Musukuma afunguka zaidi 

 

“Unakuta wasanii wetu wa bongo movie hawana kitu, sasa hivi wanategemea misiba wapate michango na kufungua madanguro na kuwa makuwadi kwa wanaume. Wako hoi bin taaban, kwa nini!? Tumeruhusu vitu vya kijinga ambavyo imetupa kabisa tasnia ya filamu. Hakuna Mtanzania anayeangalia bongo movie, Mheshimiwa waziri nusuru wasanii wanakufia mikononi mwako”, amesema Musukuma.

Pia Mbunge musukuma ameitaka wizara kulegeza masharti yaliyowekwa kwenyekusajili filamu za Tanzania na ukaguzi wake, ili kuinua sekta ya filamu ambayo hapo awali ilikuwa ikifanya vizuri.
“Ukiitoa filamu ya kibongo ina ukaguzi zaidi ya elfu moja, lakini zikija za kikorea haina ukaguzi, mmewaambia watanzania wavae madera wavae kanzu, lakini wa kikorea watu wamepiga min skirt, watu wataenda kuangalia za min skirt”, amesema Musukuma