"Nam-miss sana Zuu"- Barnaba

Wednesday , 13th Sep , 2017

Mwalimu na mwanamuziki wa bongo Fleva, Barnaba Elias 'Barnaba Classic' amefunguka na kudai anam-miss sana mama Steve 'Zuu Namela' japokuwa kwa sasa hayupo tayari kumrudia mzazi mwenzake huyo.

Msanii Barnaba akiwa na mama Steve 'Zuu Namela' enzi hizo mapenzi yakiwa moto moto kabla ya kuachana kwao.

Barnaba ameeleza hayo baada ya kupita muda mrefu tokea aachane na mzazi mwenzake huyo na kupelekea kuwa single mpaka kipindi hiki.

"Sitaweza kurudiana na mama watoto wangu japo nam-miss sana", amesema Barnaba.

Aidha, Barnaba amesema kwa upande wake mapenzi hayajawahi kumuendesha hata kidogo kama baadhi ya watu wengine wanavyokuwa baada ya kuachana na wapenzi wao kwa kushindwa hata kuendelea kufanya kazi zao.

"Niwe mkweli tu, mimi sijawahi kuendeshwa na mapenzi au mahusiano. Mapenzi hayana nafasi kubwa katika maisha yangu japokuwa yana nguvu kwa mtu yeyote yule, mapenzi hayajawahi kuchukua asilimia kubwa ya maisha yangu, kuniathiri wala kunitikisa", amesema Barnaba.

Pamoja na hayo, Barnaba ameendelea kwa kusema "Kila unachokiona kinatokea katika maisha yako kiwe kizuri au kibaya ni mapito tu, kwa sababu kilichotuleta duniani ni kingine na tunachokifanya ni kingine kwa hiyo muda mwingine kutendwa na vitu vingine ni kutenda dhambi zaidi 'so sometimes' unatakiwa upokee kwa furaha chochote utakachokumbana nacho katika maisha yako, kwa sababu hujui mpango wa Mungu ukoje. Ninachoamini mimi ni kwamba nilikuwa napita kwenye daraja ili niweze kuendela na safari aliyopanga Mungu 'so' sijui 'next' nilichopangiwa na Mwenyezi Mungu", amesisitiza Barnaba.

Kwa upande mwingine, Barnaba japo wameachana na Zuu lakini bado wanamawasiliano mazuri baina yao na kudai hivi karibuni aliongea naye kuulizia maendeleo ya Steve ya kimasomo na kumtumia pesa kwa ajili ya matumizi ya shule.